Habari

MKUTANO WA 13 WA BARAZA LA TAIFA LA BIASHARA ULIOFANYIKA TAREHE 7.6.2022 JIJINI DODOMA
  • 09 Jun, 2022
MKUTANO WA 13 WA BARAZA LA TAIFA LA BIASHARA ULIOFANYIKA TAREHE 7.6.2022 JIJINI DODOMA

RAIS na Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Biashara Mhe.  Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itaendelea kuwekeza kwenye  miundombinu wezeshi kama moja ya mkakati wa Serikali yake wa kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuvutia uwekezaji hapa nchini.

“Kuwepo kwa miundombinu wezeshi kutasaidia kujenga uchumi jumuishi sambamba na kuboresha utoaji wa huduma. Tumefanikiwa kuondoa tozo ambazo hazina tija ili kuongeza ukuaji wa biashara na uwekezaji,” amesema.

Akizungumza kwenye Mkutano wa 13 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) Jijini Dodoma, Rais Samia alisema Serikali kwa kushirikiana na Sekta Binafsi zitaendelea kufanya kazi kwa pamoja.

Kwa mujibu wa Mwnyekiti, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha kuwa Sekta za Biashara na Uwekezaji zinakuwa na kutoa mchango stahiki katika kukuza uchumi na pato la Taifa kwa manufaa ya Watanzania.

“Uboreshaji huu wa Mazingira ya Biashara uhusishe ngazi za chini pia yaani  kwenye ngazi za Wilaya na Mikoa kwani itakuwa na maana zaidi.  Tanzania ni Nchi iliyobarikiwa kuwa na rasilimali nyingi hivyo Sekta za Umma na Binafsi zinapaswa kufanya kazi kwa pamoja ili kuwaletea Watanzania maendeleo,” alisema.

Mwenyekiti aliwashukuru Wafanyabiashara kwa kuchangia fedha zilizofanikisha kutengeneza filamu ya ‘ROYAL TOUR’ ambayo imesaidia sana kuzitangaza fursa  mbalimbali ikiwemo za utalii hapa Tanzania.

“Royal Tour ni moja ya jitihada  za kimkakati zilizolenga kuvutia Watalii na Uwekezaji hapa nchini,” alisema Rais na Mwenyekiti wa Baraza Mhe.  Samia na kuongeza kuwa filamu hiyo imeshaanza kuleta matokeo chanya katika Sekta ya Utalii.

Naye Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Kattanga, Mwenyekiti wa Kamati Tendaji ya TNBC, kabla ya kumkaribisha Mwenyekiti alisema mpango wa kukuza uchumi lazima uende sambamba na kuimarisha uhusiano mzuri kati ya Sekta za Umma na Binafsi ili kufikia malengo yaliyo kusudiwa.

“Tunapenda kuwa na ‘Displined and compliant private sector’ kwani  kuanzishwa kwa ‘Blue Print’ ni moja ya hatua zilizochukuliwa kuboresha Mazingira ya kufanya Biashara na Uwekezaji,” alisema Balozi Kattanga.

Aliwataka Wafanyabiashara kujipanga kupokea wimbi kubwa la Watalii na Wawekezaji kutoka nje kutokana na  mafanikio yaliyotokana na filamu ya Royal Tour.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) na Mwakilishi wa Mwenyekiti Mwenza wa Kamati Tendaji ya TNBC, Bw Paul Makanza mbali ya kuipongeza Serikali kwa kutekeleza maazimio ya Mkutano wa 12, alisema katika kipindi kifupi cha Uongozi wa Awamu ya Sita ya Serikali ya Mhe. Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Biashara,  mafanikio mengi yamepatikana.

“Sekta Binafsi ina imani kubwa na Uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa 6 wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Baraza kwani katika kipindi cha mwaka mmoja na miezi kadhaa tumeona kukua kwa ushirikiano na kuaminiana kwa Sekta za Umma na Binafsi,” alisema.

Alishauri kuwepo kwa sera tulivu na zinazotabirika za kodi pamoja na kuwepo pia mfumo unaoeleweka wa kodi.

Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Hakuna Taarifa kwa sasa