Habari

Katibu Mkuu Kiongozi, Mwenyekiti wa Kamati Tendaji ya TNBC, aagiza taazisi za udhibiti kubadilika
  • 18 May, 2023
Katibu Mkuu Kiongozi, Mwenyekiti wa Kamati Tendaji ya TNBC,  aagiza taazisi za udhibiti kubadilika

Katibu Mkuu Kiongozi aagiza taazisi za udhibiti kubadilika

Dar es Salaam

Mei 15, 2023

SERIKALI imezielekeza taasisi zote za udhibiti hapa nchini kubadilika kifikra  na kiutendaji ili kuhamasisha na kusaidia maendeleo na ukuaji wa sekta binafsi ambayo bado ni changa na inahitaji ulezi wa serikali.

Akizungumza katika Kikao Maalum cha 43 cha Kamati Tendaji ya Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) na kuzileta pamoja Taasisi zote za Udhibiti Ikulu Dar es Salaam leo, Katibu Mkuu Kiongozi, Dr Moses Kusiluka amesema wajibu wa taasisi ni kuwezesha, kuhamasisha na kusaidia ukuaji na ustawi wa sekta binafsi na siyo kuwa kikwazo cha ukuaji wake.

Dkt. Kusiluka pia ameziagiza taasisi hizo kwenda sambamba na mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mwenyekiti wa TNBC na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuziagiza taasisi hizo kupitia changamoto zote ambazo ni kwanzo kwa ukuaji wa sekta binafsi na kupeleka mapendekezo katika Wizara husika ili zifanyiwe kazi.

Naye Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF) ambaye ni Mwenyekiti Mwenza wa Kamati Tendaji ya TNBC, Bi. Angelina Ngalula ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kufanyia kazi uboreshaji wa mifumo ya utendaji na kuongeza ufanisi kwa baadhi ya taasisi za Serikali.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza, Dkt. Godwill Wanga amesema kikao cha Kamati Tendaji cha Baraza kwa mara ya kwanza Sekta Binafsi imeipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali inazozichukua kwa kuweka mazingira mazuri ya kufanya biashara.

Kikao hicho  cha Kamati kilikuwa maalumu kwa taasisi zote za udhibiti ili kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu ajenda ya Serilika ya kuwezesha na kusaidia ukuaji wa sekta binafsi kwa maendeleo ya Taifa.