Habari
Kikao cha Kwanza cha Kikundi Kazi cha Uchumi wa Buluu chafanyika Jijini Dar es salaam
- 16 Nov, 2024

Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), limezindua kikundi kazi kwa ajili ya kuangalia fursa za kiuchumi zitakazopatikana kupitia Uchumi wa Buluu.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa kikao cha kwanza cha kikundi, Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais Abdallah Mitawi wakati wa ufunguzi wa kikao hicho kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Mitawi amesema kikundi kazi hicho ni muhimu katika kuangalia maeneo ambayo Uchumi wa Buluu utasaidia katika kukuza uchumi hapa nchini na kuchangia katika pato la taifa.
Amesema wajumbe wa kikundi hicho kutoka sekta binafsi walielezea matumaini yao ya uchangiaji wake katika ukuaji wa uchumi hapa nchini.
Mwenyekiti huyo amesema utekelezaji wa mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan baada ya mkutano wa Dunia uliofanyika mwaka 2012 Rio de Janeiro, Brazil na ule wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika mwaka 2019 ambayo kwa pamoja iliangalia mchango wa uchumi wa buluu katika kukuza uchumi barani Afrika kupitia vyanzo mbalimbali ikiwemo bahari, mito, maziwa vyenye aina mbalimbali ya samaki na viumbe wengine na mazao yanayotokana na vyanzo vya maji.
Mitawi amesema kwa upande wa Zanzibar, utekelezaji huo ulianza mwaka 2019 na tayari umepiga hatua mbalimbali ikiwemo kuanzisha Wizara maalum inayojishughulisha na uchumi wa buluu.
"Kwa Tanzania Bara, sera ya Uchumi wa Buluu tayari imeanzishwa mwaka huu na kinachofuata ni uratibu wake, ambapo Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira ndio yenye jukumu la kikatiba la kuratibu jambo hili," amesema.
Amesema utekelezaji wa Uchumi wa Buluu ni sekta mtambuka inayojumuisha sekta nyingine ikiwemo uvuvi, madini, maliasili na utalii, nishati, viwanda na biashara, uhifadhi wa mazingira, uwekezaji na umwagiliaji.
“Tumekutana ili kuangalia fursa na changamoto katika azimio hili na kuja na mapedekezo mbalimbali katika kuhakikisha sekta hii inachangia kwa kiasi kikubwa kupitia michango ya sekta nyingine hapa nchini” amesema.